BONGO MOV

AFISA UBALOZI ASIFIA JUHUDI ZA WATENGENEZAJI SINEMA YA KIBONGO READING

Fani ya utengenezaji sinema imesisitizwa kuwa moja ya misingi mikuu ya ujenzi wa maendeleo nchini.
Akizindua filamu mpya ya Lovely Gamble kwa niaba ya balozi wetu Uingereza, Amos Msanjila, aliwasifu vijana wa Urban Pulse kwa kuisaidia tasnia ughaibuni. Akiendeleza pia msamiati wa Kiswahili ofisa huyo alifafanua neno “tasnia” kuwa ni shughuli nzima ya utengenezaji sinema.

Msanjila aliyepigiwa makofi mara nyingi ndani ya ukumbi wa Wycliffe uliopambwa vyema alitaja faida kadhaa za sinema ikiwepo kutoa ajira, kusaidia jina la Tanzania kujulikana (“brand Tanzania”) na kukitangaza Kiswahili duniani.
Kiswahili kinazungumziwa na takribani watu milioni mia nne hivyo tusisahau kuwa sinema ni njia mojawapo ya kuufahamisha ulimwengu kuhusu lugha. Je, mnakumbuka enzi zile tukitazama sinema za Kihindi na kuzipenda bila hata kuelewa wanasema nini?”
Akifafanua zaidi mfano wa sinema za Kihindi na Nigeria ambazo zimependwa muda mrefu sasa alisema wao pia walianza kidogo kidogo. “Miaka ya tisini hatukufahamu sinema za Nigeria lakini leo tunazinunua. Wao pia walianzia mahali. Kidogo kidogo. Wachina wanao msemo kuwa maili elfu moja huanza na hatua chache. Hivyo  tupeane moyo iko siku  nasi tutafika.”
Mbali na sinema hii Msanjila alitaja faida za mchango wa fadhila uliofanywa na tukio. Mauzo na bidhaa za sinema (muziki na DVD) , msosi na vinywaji vilivyouzwa VItasaidia watoto yatima ambao wazazi wao walikumbwa na UKIMWI Tanzania na hapo hapo Reading.

Msanjila alisema vitendo vinavyosaidia maendeleo nyumbani kama hiki huwafanya wananchi nyumbani wawaheshimu zaidi raia wanaoishi ughaibuni.
Lovely Gamble iiliyowashirikisha waigizaji kutoka Bongo, Kenya na Uingereza inayo pia mwigizaji maarufu wa Tanzania, Steve Kanumba. Ni mchezo wa Kiswahili na Kiingereza unaoelezea mapenzi, usaliti na kushirikisha wanamuziki mbalimbali chipukizi wakiwemo wana Bongo Flava, Chemicali Ali, Andrew Mkazuzu, fundi mitambo na mtunzi Josh Mbajo.
Sinema iliyoandikwa kwa ushirikiano wa wana Urban Pulse imeongozwa na Mkenya Rennison Okemwa aliyeigiza pia, mpigaji picha kabambe toka Bongo, Baraka Baraka.

Amos Msanjila (kulia) akiwa na wageni wenzake rasmi , John Lusingu (Mwenyekiti wa Chama cha Watanzania, kushoto) wakitazama vipande vipande vya sinema ya Lovely Gamble iliyoonyeshwa baada ya hotuba kadhaa…(Picha na Baraka Baraka).
Akizungumza nami baada ya tukio la Jumamosi mwana Urban Pulse mwingine, Frank Eyembe alisema juhudi zimekamilika kutokana na ushirikiano wa vijana hawa. Ushirikiano huo umewahusisha pia wazawa wa visiwa vya Caribbean, Mark Forde na Tim Registord ambao wote wanazo taaluma mbalimbali za kisanii na kiutendeaji.
Wazungumzaji wengine waliotoa hoja ni pamoja na mwanahabari, Ayoub Mzee aliyeongelea redio mpya aliyoianzisha na kuwataka pia wapambe wasisite kutuma maoni na habari katika kipindi chake cha Swahili Diaries kinachotolewa mara moja kwa juma na Ben TV, London.
Mwanahabari mwingine kutoka Africans in London TV (AilTV) , Justina George, aliyekuwa pia mchangamshaji wa shughuli aliurudia mwito wa Balozi anayehamia Marekani mwezi huu, Mama Mwanaidi Maajar, kupendana na kushirikiana badala ya kuonena chuki na wivu. Na kwamba tukikosoana tukosoane kwa kitaaluma badala ya majungu majungu.
“Jamani tupendane…” alisema Justina kwa hamasa.